Download Mp3 from African

Je Ali Kiba hatorudia makosa yake?

Cinderella ni album yake ya kwanza ambayo ilitoka mwaka 2007, na album hii ilikuwa na nyimbo nyingi ambazo ni wazi hakuna mpenda muziki wa kizazi kipya ambae hakupata kujua nyimbo hizo.

Wimbo kama Cinderella, Mac Muga, Nichumu, Nakshi Mrembo, Njiwa, Nalia, pamoja na nyingine nyingi. Hakika hii ni wazi ilikuwa ni moja kati ya zile album bora za muda ule mpaka sasa.

Huwezi kuacha kusema Ali Kiba ni msanii mwenye kipaji cha hali ya juu, maana katika muziki wa kizazi kipya wapo wasanii ambao ni wazugaji tu ila tunawasikia kila leo katika vyombo vya habari, lakini kusikika kwao ni urafiki zaidi na sio kazi wala vipaji vya kweli.

Ali Kiba sio msanii mwenye kipaji cha uzugaji, ni kweli ana kipaji chenye maana halisi ya kipaji hasa katika muziki.

Jina la Ali Kiba lilizidi kuimarika miaka ya 2010 kabla ya miaka michache mbele kuporomoka kwa kiwango ambacho wengi iliwashangaza. Lakini Ali Kiba hakusita kuweka wazi kushuka kwake kimuziki mara baada ya kurudi na wimbo wa mwana ambapo alisema “Niliamua kuwa kimya na si kama nilishindwa muziki, isipokuwa kuwa na karibu na watoto wangu hasa katika malezi. Ila sasa nimerudi na hakika kiti changu nilichokaa kina vumbi hivyo nafuta tu na kuketi”

Hakika ameketi na tunaona ukubwa wake katika muziki wa bongo fleva.

Moja kati ya wasanii walipaswa kuwa mbali zaidi katika muziki wa bongo fleva ni Ali Kiba. Kasumba kubwa ya mashabiki wa muziki hasa wa kizazi cha Instagram ni kutokujua nani alifanya nini kabla mtandao wa picha Instagram. Na ni wazi wala sio kificho mashabiki hawa wamekuwa wajuaji zaidi lakini kiuhalisia si mashabiki wenye kujua muziki bali wengi wao ni bendera fuata upepo.

Jambo jema ni kukumbushana yaliyopita kabla tuliyonayo hayajaharibika na kuondoka kabisa.

Mwaka 2010-2011 msanii Ali Kiba alishirikia katika mradi wa One 8 kampeni ambayo ailishirikisha wakali kama 2face Idibia, Fally Ipupa, Amani, Navio, Jk, na Movaizhaleine. Ambapo mradi huu ulifanyika kwa kutengeneza wimbo wa pamoja ambao ni wimbo uliondikwa na Robert Kelly maarufu kama R.Kelly, ambaye pia ndiye alikyekuwa msimamizi wa kuingiza sauti na hata katika uchukuaji wa utengenezaji video.

Hakika Ali Kiba alionyesha uwezo wa hali ya juu, na hata kuwa moja kati ya wasanii watatu ambao waliweka sauti za nyuma ya wimbo huo. Amani alikuwa ni mmoja wa msanii walioweka sauti za nyuma katika wimbo huo. Lakini R Kelly pia aliweka, licha ya sauti ya kiba kusikika mara nyingi katika wimbo huo.

Ni wazi kila mpenda muziki wa kizazi kipya hakuwa na lakusema vibaya isipokuwa kusifu uwezo alionyesha Ali Kiba mbele ya wasanii walio wengi na wenye vipaji vya hali ya juu tokea Afrika.

Hakika Ali Kiba hakuwa mbinafsi kueleza mengi mazuri ambayo alijifunza wakati wa ufanyaji wa mradi huo One 8. Moja kati ya mambo mema ambayo aliweka wazo ilikuwa ni “R Kelly ametupa nafasi ya kumtumia kufanya kazi na yeye au msanii yoyote yule wa Marekani”

Ni wazi Ali Kiba hakuwahi kutumia kwa vitendo kauli hiyo, zaidi ya kuingia shimoni na kuendelea kuwepo katika ushirikishwaji wa wasanii wengi wa bongo fleva. Huwezi kuacha kusema kuwa haya yalikuwa makosa kwa kutokutumia nafasi ambayo ni wazi ilikuwa wazi kutoka kwa mkongwe R.Kelly.

Hii ilinifanya nione Ali Kiba sio msanii ambaye anataka kwenda mbele zaidi, na hata kuona ni msanii mwenye kuridhika na soko la bongo lililojaa majungu, kujuana, umbea na hata kupeana nafasi kwa upendeleo zaidi.

Msemo wa” Bahati haiji mara mbili” umeshindwa kufanya kazi mbele ya Ali Kiba. Ambapo mapema mwaka huu 2016 imekuwa bahati kwake kwa kusainiwa na kampuni ya Sony ambapo atakuwa chini na uongozi mmoja na msanii Chris Brown,John Legend, na Davido. Hili ni jambo jema zaidi katika muziki wa bongo fleva, lakini ikumbukwe hata Rose Mhando ambaye ni msanii wa nyimbo za dini alisainiwa miaka kadhaa ya nyuma lakini hatukupata kuona tena utendaji wake ukilinganisha kabla ya yeye kusainiwa na sony.

Naamini katika kipaji cha Ali Kiba, sitaki kuamini kama atarudia makosa aliyofanya mwaka 2010-2011. Lakini katika ukubwa alionao sasa nategemea akiwa na kundi kubwa la watu katika ufanyaji wa kazi zake na sio kuwa kama yeye tu kama ilivyosasa.

Lakini je Ali Kiba hatorudia makosa yake?
Tag : lainnya
Back To Top