Download Mp3 from African

Wamachinga wapewa siku vii kuondoa biashara barabarani

MANISPAA ya Dodoma imetoa siku saba kwa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu ‘machinga’ wanaopanga bidhaa zao kando kando ya barabara, kuziondoa.


Amri hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, wakati akizungumza na wafanyabiashara katika kituo kikuu cha mabasi mkoani humo.

Kunambi alisema baadhi ya wafanyabiashara, walikuwa wakikataa kufanya biashara ndani ya soko, badala yake wanapanga chini.

Alisema masoko mengi yapo wazi, lakini baadhi yao wanafanya biashara maeneo yaliyokatazwa na kuvunja sheria.

“Wanaopanga biashara zao kando ya barabara, lazima waondoke ndani ya siku saba zijazo kuanzia sasa, masoko yapo na tunataka mji huu uwe safi,” alisema.

Alisema atapitisha fagio la chuma kwa watakaokaidi agizo hilo, kwa kuwa masoko mengi yapo wazi kutokana na kuyakimbia na kujazana kando ya barabara, hali inayowapa shida wanaopita kwa miguu.

Aidha, alisema kuanzia sasa manispaa hiyo itawachukulia hatua kali watakaobainika kutupa taka ovyo, kwa kuwa wameandaa vijana wa operesheni maalumu ya kuiweka manispaa safi.

“Ukikamatwa unatupa takataka ovyo, tunakupeleka mahakamani ili adhabu ikukute,” alisema.

Aliwataka wananchi wa manispaa hiyo, kuhakikisha mazingira ya nyumba zao yanakuwa safi.

Alisema pamoja na maagizo hayo, pia manispaa yake inapiga marufuku ubandikaji ovyo wa matangazo kwenye kuta ama nguzo, yanayosababisha uchafu kwenye mji.
Tag : lainnya
Back To Top