Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara CBE wakivaa kofia zao mara baada ya kutunukiwa Shahada zao katika fani mbalimbali wakati wa mahafali ya 51 ya Chuo cha Elimu ya Biashara jijini Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amewataka wahitimu 1,811 wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) waliotunukiwa stahili zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016 kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini kwa kuanzisha makampuni na viwanda vidogo vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.
Akizungumza katika mahafali ya 51 ya chuo hicho jijini Dar es salaam Mhe.Mwijage amesema kuwa makampuni na viwanda vidogo vidogo watakavyoanzisha vitatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora ambazo zitauzwa kote duniani hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuwapatia ajira ya uhakika.
Amesema Serikali ya Tanzania inapenda kuwaona Wawekezaji wengi wa Kitanzania wakiingia na kuwekeza kwenye rasilimali mbalimbali zilizopo nchini Tanzania badala ya kuwaachia wageni kwa kuwa inao wasomi waliobobea kwenye fani ya biashara pamoja na ujasiriamali.
" Taifa letu limebarikiwa kuwa na fursa nyingi za kujiletea maendeleo, Serikali ingependa kuona wawekezaji wengi wa Kitanzania wakiwekeza kwenye rasilimali zilizopo kwa mfano tunayo gesi, madini, kilimo na na rasilimali nyinginezo nyingi" Amesisitiza Mhe.Mwijage.
Amefafanua kuwa Serikali itaendelaea kuwekeza kwenye Elimu ya Biashara kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi hasa Biashara.
Tag :
lainnya