Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ana uhakika kuwa bado kuna wanachama wanaomuunga mkono ndani ya CCM na sasa anawataka waendelee kushikamana naye, kauli ambayo inaweza kuchochea moto ndani ya CCM. Katika taarifa yake fupi kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Lowassa amewahakikishia wananchi kuwa kwa sasa ana “ari, nguvu na hamasa kuliko wakati mwingine wowote”.Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alijiondoa kwenye chama tawala Julai 28 mwaka jana baada ya jina lake kuondolewa kwenye orodha ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM.
Kuondoka kwake kulisababisha mawaziri wa zamani, wabunge, wenyeviti wa mikoa, madiwani na wanachama wengine wa CCM, wakiongozwa na waziri mwingine mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kukihama chama hicho, hali iliyosababisha ushindani kuwa mkubwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, huku CCM ikilalamikia kusalitiwa. Wakati CCM ikifikiria hatua za kuchukua dhidi ya wasaliti wa chama wanaotuhumiwa kuunga mkono harakati za upinzani wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Lowassa ameongeza petroli kwenye moto ulioanza kuwaka.
“Kwa wale wenzangu waliobaki CCM na wanaoniunga mkono, tuendelee kushikamana na kunipatia taarifa kwa hatima ya nchi yetu,”amesema Lowassa ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
“Nawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na wenzangu ndani Chadema.”
Tag :
lainnya