VITENDO vya ukatili wa kijinsia na dhuluma dhidi ya watoto wa kike vimekuwa vikishamiri kila siku pamoja na kuwepo kwa taasisi za kutetea haki za wanawake na kuanzishwa kwa madawati ya Kijinsia kwenye vituo vya polisi nchini.
Msichana wa kidato cha Nne mwenye umri wa miaka 17,(jina tunalo) anayesoma shule moja ya sekondari ya Kata mkoani Mbeya amekumbwa na kadhia ya kuvuliwa nguo zake za ndani na kucharazwa bakora zisizo na idadi na walimu wanne wa shule hiyo.
Tukio hilo ambalo limeripotiwa katika kituo kidogo cha Polisi Mbalizi wilaya ya Mbeya kwenye jalada la uchunguzi namba MBI/IR/967/2016na kuwekwa kwenye taarifa yenye namba MBI/RB/2653/2016 linadaiwa kuwahusisha walimu wanne akiwemo Mkuu wa shule hiyo pamoja na walimu watatu.
Akizungumza huku akiwa na maumivu makali katika Hospitali Teule ya Ifisi ambako amelazwa akipatiwa matibabu, mwanafunzi huyo alisema kuwa aliitwa na mwalimu wa nidhamu aliyemtaja kwa jina la Neema Mwaikenda aliyekuwa pamoja na Mkuu wa shule hiyo aliyemtaja kwa jina la Mariamu Mwanisenga na mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili.
Alisema walimu hao walianza kumuadhibu kwa viboko visivyo na idadi huku akiwa amechojolewa nguo zake ambapo mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili akaanza kumshikashika sehemu zake za siri.
‘’Wakati naadhibiwa na walimu wote, huyu mwalimu wa kiume alianza kunishika huku chini,na kunitaka niwataje wanaume zangu,nikawa nabana miguu wakazidi kunishambulia kwa vibao na mateke na fimbo,’’alisema mwanafunzi huyo.
Tag :
lainnya